Historia ya Roselyne Swai – maono na motisha


 

 

 

 

Jina langu ni Roselyne Swai. Nina umri wa miaka 50. Mimi ni mwanzilishi wa kituo cha Rose Education Centre.

Nilipokuwa nina umri wa miaka miwili, niliugua surua na tetekuwanga kwa pamoja. Nilipata matibabu ya sindano zilizosababisha miguu yangu yote miwili kupooza. Sikuweza kutembea tena zaidi ya kutambaa kwa mikono. Wazazi wangu walijaribu kunipa mazoezi na kunipeleka hospitali tofauti tofauti bila ya mafanikio. Niliishia kuwa mlemavu wa miguu.

Roselyne-Swai-mkurugenzi


Nilipokuwa na umri wa miaka 11, baba yangu mzazi alipata ajali ya gari na kufariki dunia hapo hapo. Mama yangu mzazi hakuwa na uwezo wa kunipeleka shule ya kulala. Alijaribu kutafuta misaada hasa katika kanisa alilokuwa anasali.

Kwa bahati nzuri alifanikiwa kupata padri wa kizungu aliyetokea nchini Uingereza ambaye alikuwa ni kiongozi wa kanisa la katoliki. Padri huyu alijitolea kunifadhili elimu ya shule ya kulala na mahitaji mengine yote.

Hivyo nilifanikiwa kupata elimu. Hii ilinipa furaha kubwa. Baada ya kumaliza elimu yangu, nilikuwa na ndoto za kusaidia watoto wenye ulemavu, watoto wa mitaani na watoto wanaotoka katika mazingira magumu. Hii ni kwa sababu, mtoto akipata nafasi ya kusoma na akawa msomi atakuwa na fursa ya kupata kazi nzuri na kujikwamua kiuchumi. Mimi binafsi nilipata elimu na nimeweza kujikwamua kiuchumi na kubadilisha muelekeo wa maisha yangu. Nilipata msaada kwa wafadhili mbali mbali.

Nilianza kwa kufungua kituo cha kufundisha wanafunzi wa madarasa tofauti yakiwemo sekondari. Wanafunzi hawa walitokea shule mbali mbali na hivyo niliwafundisha nyakati za jioni kila siku. Wazazi wao walinilipa pesa kidogo ambazo nilikuwa nahifadhi ili kupata mtaji mkubwa.

Kuzaliwa kwa Rose Education Centre

Kazi hii ilikuwa ngumu kwangu kutokana na udogo wa sehemu ya kufundishia. Kwani nilianza kufundishia katika chumba changu kidogo nilichokuwa nimepanga na nilikiita kituo changu Rose Education Centre.

Wanafunzi walikaa kwenye kitanda changu kidogo na walinisikiliza nikiwa mbele yao nimekaa kwenye kiti changu. Nilitumia vipande vidogo vya mbao na vipande vya maboksi kuandikia na wanafunzi pia walitumia kunakili notes walizokuwa wanaandika.

Idadi ya wanafunzi iliongezeka kutoka wanafunzi watatu waliokuwa wameanza mpaka kufikia 18 ndani ya miezi mitatu. Sikuwa na vitabu vya kufundishia. Hivyo ilinipasa mimi kuwa mwanachama wa Maktaba ya mkoa ili niweze kuazima vitabu kwa ajili ya kufundishia mpaka hapo nilivyoweza kununua vitabu vyangu.

Malengo yangu ya kufungua kituo pamoja na shule yalikuwa yanagonga katika akili yangu usiku na mchana. Nilihitaji kusaidia watoto wenye shida mbalimbali kama walemavu, yatima, na wanaotoka kwenye familia masikini kwa kuanzisha shule ya chekechea na hata shule ya msingi. Nilifikiria sana ni jinsi gani nitaweza kupata fedha za kununua eneo kubwa la kujenga shule na kituo cha watoto yatima. Kujenga kituo cha watoto yatima na kujenga shule ilihitaji fedha nyingi za kitanzania. Milioni nyingi za fedha. Nilihitaji eneo linalozidi ekari tano, ili niweze kujenga hosteli ya watoto ya kulala, iwe na eneo la michezo na eneo kubwa la kujenga madarasa. Nilihitaji vitanda, magodoro, vyombo vya jikoni, makabati ya kuhifadhi vitabu, vifaa vya ufundishaji kama vitabu, kalamu, vifaa vya michezo na aina nyingi ya vifaa vya shule na kituo.

Niliacha kufundisha watoto masomo ya jioni kwa wanafunzi wanaotoka shule mbalimbali za msingi na sekondari baada ya kufundisha kwa miaka mitano, kutoka mwaka 1997 – 2003. Nilifanya maamuzi haya ya kutofundisha watoto masomo ya jioni kwa sababu nilihitaji kufungua shule mpya ya kudumu ya chekechea na shule ya msingi.

Huu ukawa mwanzo wa uanzilishi wa shule ya Rose Education Centre.