Mwaka 2003, nilijaribu kukodisha nyumba ndogo na katika hiyo nyumba nilifungua shule ya chekechea. Nilianza na wanafunzi 8 na mwishoni mwaka 2003 nilifanikiwa kupata wanafunzi 25 waliofuzu kuingia darasa la saba mwaka 2004.
Mwaka huo huo wa 2004, nilipangisha nyumba maeneo ya Majengo Moshi mjini yenye vyumba 6, uwanja mdogo wa kuchezea, uzio wenye mlango mkuu wa kuingilia maji na umeme. Niliweka michezo ya nje kwa watoto kama kubembea na kuruka huku na kule. Nilinunua vifaa mbalimbali vya michezo ya ndani kwa ajili ya chekechea.
Nilihakikisha kuwa wanafunzi wanapata uji wa asubuhi hivyo ilinipasa kununua vyombo vya jikoni kama vijiko, vikombe, majiko ya kupikia, sufuria na vifaa vengine mbali mbali vya jikoni. Niliajiri walimu wawili na mpishi mmoja. Kila mwaka nilipata wanafunzi wanaotoka katika mazingira magumu kama watoto wa mtaani, yatima na wale wanaotoka kwenye familia za kimasikini. Wanafunzi hawa walihitaji msaada wa elimu, chakula na mavazi.
Ili kuanza shule ya binafsi, Serikali ya Tanzania inahitaji shule kuwa na namba ya usajili. Hivyo nilianza kufatilia taratibu za kupata usajili zilizokuwa zinahitajika. Kwa sababu Serikali ya Tanzania hairuhusu kuendesha shule katika nyumba za kupanga, ilinilazimu kununua Kiwanja kikubwa ili kuweza kujenga majengo ya kudumu ya shule. Kiwanja hiki nilinunua katika kijiji cha Mtakuja kata ya Mabogini upande wa Moshi vijijini. Hii ilikuwa mwaka 2006.
Ujenzi wa shule
Miaka miwili baadaye, kwenye mwaka 2008, nilipata ruhusa kutoka serikalini kujenga shule ya chekechea na ya msingi.
Lengo langu kubwa ni kuwa na shule bora ya mchepuo wa kingereza na ya kisasa.
Mwaka 2009, kabla sijahamisha kituo changu na shule yangu kutokea Majengo – Moshi mjini na kuhamia Mtakuja, shule ilikuwa na wanafunzi 73 wakiwemo yatima 17. Wanafunzi wa chekechea walikuwa 25 na wanafunzi wa shule ya msingi walikuwa 48.
Siku ya leo
Leo, shule ya Rose Education Centre imepata maendeleo makubwa kwa shule ya chekechea na shule ya msingi ikiwa ni shule ya kutwa na ya kulala. Mahitaji ya shule yakiwemo vyumba zaidi ya 12 vya madarasa, ofisi za walimu, bwawa la chakula na jengo la utawala. Mabweni makubwa 2 kwa wasichana na wavulana.
Shule ina ulinzi wa hali ya juu. Kwani iko na ukuta mrefu uliozunguka shule na pia mlango mkubwa wa kuingilia shuleni, akiwepo mlinzi mlangoni kuweka usalama wa watoto ulio wa uhakika.
Nilijikusanyia kiasi cha fedha kilichotosha kununua eneo la ekari nane na kuanza ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na bweni la watoto wa kiume. Pia nilijenga vyumba vitatu vya madarasa kwa kutumia vipande vya mbao. Bado ujenzi ulikuwa mgumu sana kwangu.